6 January 2015

AKAMATWA NA MIL.400/-FEKI MWANZA

njiwa

 
JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia mkazi wa Buzuruga jijini hapa, Zakaria Matiku Werema (35) baada ya kukamatwa akiwa na fedha bandia za Tanzania na za kigeni, ambazo kama zingekuwa halali zingekuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 400.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 2, mwaka huu, majira ya saa 8:00 alipokuwa kwenye harakati za kutafuta wateja.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kwenye mtaa wa Rwegasore wilaya ya Nyamagana jijini hapa akiwa na noti bandia za Sh elfu tano tano zenye thamani ya Sh 11,955,000, ambazo alizificha ndani ya kasha dogo la kuhifadhia glasi na kulivisha mfuko mweusi.
Alisema mtuhumiwa baada ya kukamatwa, askari walikwenda naye nyumbani kwake Buzuruga kwa ajili ya upekuzi, ambako walifanikiwa kumkuta na dola bandia za Marekani 244,100 sawa na Sh 414, 970,000 za Tanzania na fedha bandia za Tanzania Sh 12,000,000 ambazo alizificha kwenye kona chumbani kwake.
“Mtuhumiwa tulimkamata akiwa na fedha bandia Shilingi 23,955,000 na dola bandia za Marekani 244,100, kama fedha hizo zote zingekuwa ni halali zingekuwa na thamani ya Shilingi 438,925,000, endapo zingeingia kwenye mzunguko zingesababisha madhara makubwa na ni wazi uchumi wa nchi yetu ungeyumba,” alisema Kamanda huyo.
Aliongeza kuwa walipomfanyia mahojiano, mtuhumiwa alikiri kununua fedha zote hizo eneo la Isibania nchini Kenya Desemba 22, mwaka jana, kwa thamani ya Sh milioni nane za Tanzania.
Alisema mtuhumiwa aliingiza fedha hizo bandia nchini kwa ajili ya kuziuza na kwamba alipanga kuuza Sh 300,000 halali kwa Sh 1,000,000 bandia na dola moja alipanga kuiza kwa Sh 800 ya Tanzania.
Polisi wanaendelea kumhoji ili kubaini na kuuvunja mtandao wote, unaojihusisha na biashara hiyo haramu. Kamanda Mlowola alitoa rai kwa wafanyabiashara wa jiji na mkoani hapa kuwa waangalifu wanapofanya miamala ya fedha za kigeni na pia watilie shaka pale wanapouziwa fedha za kigeni kwa bei ya chini.
njiwa2

Like Page Yetu Hapa Kuungana Nasi Facebook